KUFANYA IBADA YA KWELI NI MAAMUZI, SIO YA HISIA.
Katika Matendo 16:25–31, tunaona mojawapo ya mifano yenye nguvu zaidi ya kuabudu katika mateso. Mtume Paulo na Sila walipigwa, walisingiziwa, na kutupwa gerezani. Miguu yao ilifungwa kwa mkatale. Ilikuwa ni maumivu. Ilikuwa ni dhuluma. Ilikuwa ni usiku wa manane—saa ya giza nene zaidi.
Hata hivyo, badala ya kulalamika, waliomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa.
1. IBADA YA KWELI HAITEGEMEI MAZINGIRA BALI INATEGEMEA MAAMUZI/MSIMAMO (IMANI). MATENDO 16:25-31, YOHANA 4:23
Matendo 16:25 “Lakini karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kumwimbia Mungu nyimbo za sifa…
Yohana 4:23 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. hao wamwabudu awatafuta watu kama hao wamwabudu
Haya ni matokeo ya moyo uliogeuzwa kwa ajili ya kusudi Lake.
Usiku wa manane unawakilisha:
o Majira ya giza totoro.
o Kuchanganyikiwa na kutokuwa na uhakika.
o Maumivu na upweke.
Hawakusubiri asubuhi. Hawakusubiri uhuru. Walichagua kuabudu katikati ya dhoruba.
Ibada ya kweli haitegemei mazingira bali msimamo wa moyo.
Tunapoabudu katika majaribu, tunatangaza kwamba Mungu bado anastahili.
2. IBADA YAKO YA KWELI INAWAGUSA WENGINE. Matendo 16:25
“…na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.”
• Mateso yao yakawa ushuhuda.
• Gereza lao likawa patakatifu.
• Maumivu yao yakawa jukwaa la huduma.
Watu wanatazama jinsi tunavyoitikia katika majira magumu. Ibada yako wakati wa majaribu inaweza:
• Kuwatia wengine moyo.
• Kuwaulisha waumini walio dhaifu.
• Kuwavuta wasioamini karibu na Mungu.
3. IBADA YA KWELI INAMKARIBISHA MUNGU KUINGILIA KATI (INTERVENTION). Matendo 16:26, Yoshua 6:20
“Ghafula pakawa na tetemeko kuu la nchi…”
Mungu alijibu. Misingi yalitikiswa. Milango ikafunguka. Minyororo ikakatika. Kama kuta za Yeriko, misingi ya mji ilitikiswa na kuanguka.
Yoshua 6:20 “Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga sauti za tumpatu… kuta za mji zikaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu wakaingia katika mji…”
2 Mambo ya Nyakati 20:21
“Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele.” “Hata walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri… nao wakapigwa.”
Ibada ya KWELI:
• Inatikisa misingi ya Adui.
• Inafungua milango iliyofungwa.
• Inakata minyororo ya yule mwovu.
Sio kila wakati wa ibada huleta tetemeko la ardhi, lakini kila wakati wa ibada ya kweli hualika uwepo na nguvu za Mungu. Ibada ya kweli si burudani; ni uzoefu hai wa mabadiliko katika uwepo wa Mungu. Inatutoa kwenye kuwa watazamaji wanaoburudika na kutufanya washiriki tuliogeuzwa katika uwepo wa Mungu.
4. IBADA KWELI HUPELEKEA WATU KUPOKEA WOKOVU. Matendo 16:27-31
Mlinzi wa gereza alikuwa karibu kujiua. Alidhani kila kitu kimepotea. Lakini Paulo akapiga kelele, “Usijidhuru!” Ibada yao haikuwafanya wawe huru pekee—iliokoa familia. Mlinzi aliuliza:
“Nifanye nini nipate kuokoka?” Walijibu: “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka, pamoja na nyumba yako.”
Ibada yao ya usiku wa manane ilizaa:
• Moyo uliogeuzwa.
• Kaya (familia) iliokolewa.
• Hali iliyobadilika kabisa.
HITIMISHO
Chochote unachopitia sasa hivi, kisinyamazishe sifa zako mbele za Mungu. Minyororo yako inaweza kuwa ya kimwili, kihisia, kifedha, au kiroho—lakini ibada bado inafanya kazi.
• Hata gerezani, Mungu yupo.
• Hata kwenye giza au gizani, Mungu ana nguvu.
• Hata katika majaribu, Mungu anastahili.






